Dodoma FM

J1 wagusa maisha ya watoto wenye uhitaji Dodoma

21 September 2026, 16:31

Pichani Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma waliotimiza miaka kumi ya utumishi, maarufu kama J1 wakitio msaada kwa watoto wenye uhitaji. Picha na Mwandishi wetu.

Tukio hilo limekuwa sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuimarisha uhusiano na jamii, huku Umoja wa Askari J1 ukiendelea kutumia maadhimisho yao kama fursa ya kugusa maisha ya wenye uhitaji.

Na Anwary Shabani.

Umoja wa Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma waliotimiza miaka kumi ya utumishi, maarufu kama J1, umeadhimisha miaka hiyo kwa kufanya matendo ya huruma kwa watoto wenye uhitaji katika Kituo cha Tupendane, kilichopo Kikuyu jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Dodoma, ASP Regina Mtana, amesema Jeshi la Polisi ni sehemu ya jamii na lina wajibu wa kushirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kijamii.

ASP Mtana amesema msaada huo umetolewa na askari hao kwa kutumia sehemu ya kipato chao, ukiwa na lengo la kuwasaidia watoto kupata mahitaji muhimu, kurejesha faraja na kuwawezesha kuendelea vizuri na masomo yao.

Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Askari Namba J1 Mkoa wa Dodoma, James Boymanda, amesema umoja huo umekuwa na utaratibu wa kufanya shughuli za kijamii mara kwa mara, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha umoja na mshikamano, pamoja na kuwasaidia watoto wenye uhitaji kufikia malengo yao.

Naye Mwakilishi wa Kituo cha Tupendane, Fatma Mgeni, amelishukuru Jeshi la Polisi kupitia Umoja wa Askari J1 kwa kukumbuka jamii katika maadhimisho hayo, akisema msaada huo umesaidia kupunguza changamoto ya baadhi ya mahitaji, ikiwemo vifaa vya shule.

Simulizi na Anwary Shabani.