Dodoma FM

NEST yarahisisha mfumo wa zabuni nchini

20 August 2026, 16:48

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, PPRA, Dennis Kwame Simba.Picha na Anwary Shaban.

Hatua hiyo inaonesha namna matumizi ya teknolojia katika ununuzi wa umma yanavyoweza kupunguza gharama, kuokoa muda na kuongeza fursa kwa wazabuni kushiriki katika zabuni za Serikali bila vikwazo vya umbali.

Na Anwary Shaban.

Matumizi ya Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya kielektroniki, NEST, yameendelea kuleta matokeo katika kupunguza gharama za uendeshaji wa zabuni nchini, ambapo zaidi ya karatasi milioni 288.6 za nyaraka za zabuni zimezuiwa kuchapishwa, hatua iliyosaidia kuokoa takriban shilingi bilioni 27.64.

Akizungumza katika ofisi za Habari Maelezo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, PPRA, Dennis Kwame Simba, amesema matumizi ya mfumo huo yameondoa ulazima kwa wazabuni kusafiri kupeleka nyaraka za zabuni katika taasisi zinazonunua, hivyo kupunguza gharama na muda wa kushiriki katika michakato ya ununuzi wa umma.

Amesema mfumo huo pia umewawezesha wazabuni kuomba zabuni wakiwa katika maeneo mbalimbali bila kulazimika kufika katika taasisi husika.

Sauti ya Dennis Kwame Simba.

Aidha, Simba amesema PPRA inaendelea na utafiti kuhusu fursa za biashara ya kaboni, ambapo mfumo wa NEST tayari umesajiliwa ili kuingia katika biashara hiyo, hatua inayotarajiwa kuchangia takriban shilingi bilioni 20 kwa mwaka kupitia mauzo ya kaboni.

Kwa upande wake, Elizabeth Kasimila, ambaye ni mmoja wa mashuhuda wa matumizi ya mfumo wa NEST, amesema mfumo huo umewasaidia wao kama kundi la kazi kupata zabuni 21 kutoka katika wizara mbalimbali za Serikali, zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.196.

Sauti ya Elizabeth Kasimila,