Dodoma FM

Wananchi Msagali wachangia milioni 48 ujenzi wa kituo cha afya

17 September 2026, 16:50

Pichani katibu wa kamati ya ujenzi Bw Samwel Mtafu na baadhi ya wananchi katika kuhakikisha ujenzi wa zahanati inafanikiwa. Picha na Steven Noel.

Wananchi hao wameendelea kuiomba Serikali, viongozi na wadau wa maendeleo kushirikiana nao katika kukamilisha ujenzi huo, wakisema hatua hiyo itakuwa muhimu katika kuboresha huduma za afya katika Kijiji cha Msagali na maeneo ya jirani.

Na Stephen Noel.

Wananchi wa Kijiji cha Msagali, Kata ya Chunyu, Wilaya ya Mpwapwa, wameamua kujikwamua kwa kuchangisha fedha na kuanza ujenzi wa kituo cha afya, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya, hususani wakati wa msimu wa mvua, pamoja na kusaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi hao kukabiliwa kwa muda mrefu na changamoto ya usafiri na miundombinu ya barabara, hali ambayo huwafanya kupata ugumu wa kuwafikisha wagonjwa katika vituo vya afya kwa wakati, hasa wakati wa masika.

Wakizungumza na Dodoma FM katika mahojiano maalum yaliyofanyika kijijini hapo, Matayo Mtafu na Raheki Chalo, pamoja na Katibu wa Kamati ya Ujenzi wa Kituo hicho, Samweli Mtafu, wamesema changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi wakati wa mvua ambapo baadhi ya maeneo ya kijiji huwa magumu kupitika.

Samweli Mtafu amesema hadi kufikia hatua ya ujenzi wa lenta, wananchi wamefanikiwa kuchangisha jumla ya shilingi 48,560,000, huku akiiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza na kusaidia fedha na vifaa ili kukamilisha ujenzi huo.

Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia wananchi kupata huduma za afya kwa urahisi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu, hasa katika kipindi ambacho barabara huwa hazipitiki kwa urahisi.

Kwa upande wake, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Chunyu, Jonathan Lusinde, amesema Kijiji hicho kina wakazi wapatao 19,190, ambao wanatarajiwa kunufaika na huduma za afya zitakazotolewa katika kituo hicho mara kitakapokamilika.

Naye Manga Mfawidhi wa zahanati hiyo amesema kituo hicho cha sasa kinakabiliwa na ongezeko la idadi ya wagonjwa, akieleza kuwa kwa mwezi mmoja zahanati hiyo huhudumia takribani wagonjwa wa nje 1,200.

Amesema kukamilika kwa kituo hicho cha afya kutapunguza mzigo wa wagonjwa katika zahanati hiyo na kuongeza uwezo wa wananchi kupata huduma za afya kwa wakati, hususani akina mama wajawazito na watoto.

Ripoti ya Stephen Noel.