Dodoma FM

Waajiri watakiwa kujenga utamaduni wa kupima wafanyakazi afya ya akili

11 September 2026, 16:15

Changamoto mbalimbali za kisaikolojia zisipotambuliwa na kushughulikiwa mapema, zinaweza kuathiri utendaji kazi. Picha na mtandao.

Wataalamu wa afya ya akili wanasisitiza kuwa kutambua mapema mabadiliko ya tabia, hisia na mwenendo wa mfanyakazi ni hatua muhimu katika kumsaidia kabla changamoto haijawa kubwa. Hivyo, mazingira ya kazi yanapaswa kuwa sehemu salama ya wafanyakazi kuzungumza kuhusu changamoto zao na kupata msaada unaohitajika kwa wakati.

Na Anwary Shabani.

Waajiri na wafanyakazi katika taasisi za umma na binafsi wametakiwa  kujenga utamaduni wa kutambua viashiria vya changamoto za afya ya akili miongoni mwa wafanyakazi, ili hatua za haraka zichukuliwe kabla hali hiyo haijawa kubwa na kusababisha madhara zaidi, ikiwemo mtu kufikia hatua ya kujitoa uhai.

Wito huo umetolewa na Msaikolojia kutoka Taasisi ya Afya ya Akili Tanzania, Dkt. Arapha Arajiga, ambaye amesema uelewa wa viashiria vya changamoto za afya ya akili ni muhimu kwa kila mfanyakazi, kwa kuwa changamoto hizo zinaweza kumpata mtu akiwa kazini au hata katika mazingira ya familia.

Dkt. Arajiga amesema baadhi ya wafanyakazi hupitia changamoto mbalimbali za kisaikolojia ambazo, zisipotambuliwa na kushughulikiwa mapema, zinaweza kuathiri utendaji wao wa kazi, mahusiano na maisha yao kwa ujumla.

Kwa upande wake, Afisa Mkaguzi wa Uhamiaji kutoka Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Joseph Mgoba, amesema kitengo hicho kimekuwa kikichukua hatua mbalimbali kumsaidia mfanyakazi anayebainika kuwa na changamoto ya afya ya akili, ikiwa ni pamoja na kumuelekeza kwenye huduma stahiki.

Mgoba pia amewataka watu wanaopitia msongo wa mawazo au changamoto nyingine za afya ya akili kutokaa kimya, bali kuzungumza na mtu wanayemwamini na kutafuta msaada wa kitaalamu, akisisitiza kuwa kuomba ushauri ni miongoni mwa hatua muhimu za awali katika kukabiliana na changamoto hizo.

Sauti na Anwary Shabani.