Dodoma FM

KILIMO HIMILIVU NGUZO YA UZALISHAJI KWA WAKULIMA

9 August 2021, 12:44 pm

Na,Mhindi Joseph Dodoma Tanzania

Tanzania ni Miongoni mwa nchi inayokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi kwani Asilimia 1 ya pato la Taifa inatajwa kupotea kila mwaka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi huku ikikadiriwa kuwa watu milioni 1.6 wanaoishi ukanda wa pwani watakabiliwa na changamoto ya athari za mabadiliko ya tabia nchi ifikapo mwaka 2030.

Wakati huo Tanzania Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 wastani wa asilimia 2 ya pato la taifa itapotea.

Katika Mkoa wa Dodoma mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakisababisha mvua kutonyesha katika vipindi vilivyozoeleka, kuongezeka kwa joto, ukame na wakati mwingine mvua kunyesha nyingi kuliko matarajio na kusababisha mafuriko.

Hali ya hewa isiyotulia katika kalenda ya kawaida ni tishio kubwa kwa kilimo ambacho ni uti wa Mgongo kwa Watanzania, kwa kujipatia kipato.

Sehemu kubwa ya mabadiliko ya tabianchi inasababishwa na shughuli za kinabadamu ikiwemo kilimo ukataji wa miti hovyo, ikiwa miti inasaidia katika kunyonya gesi ukaa na gesi joto zinazosabaisha mabadiliko haya.

Dhana iliyopo pia ni kwamba, kilimo kisichozingatia mabadiliko ya tabianchi kinachangia kuongeza hewa gesi isiyotakiwa (green gases) na hewa ukaa kutokana na ukataji wa miti, uchomaji moto au ufugaji wa kupita kiasi.
Tafiti zilizopo zinaonesha kwamba ugeuzaji wa misitu kuwa mashamba unachangia zaidi ya asilimia 70 ya uharibifu wa misitu.

Mwandishi wa Makala hii ametembelea katika kata ya Hombolo bwawani Mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ambayo kilimo himilivu kinatumika Zaidi na wakulima katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

Gabriel alex Mwangalima ni Mkulima katika kata ya hombolo anasema kilimo Himilivu kimekuwa na tija kwake kwani kwani anauwezo wa kuzalisha gunia 6 hadi 7 wa zao Mahindi kwenye shamba la heka moja.

“Mwanzo ilikuwa inanipa ugumu wa kulima kutokana na Dodoma kuwa kame na mabadiliko ya hali ya hewa nilikuwa nikilima sipati uzalishaji wenye tija lakini kilimo himilivu kimekuwa mkombozi kwangu”
Deogratius Jamal Elikuta ni Mkulima anasema Kilimo himilivu kimememsaidia kuwa na uzalishaji wa juu.

“Mwanzo nilikuwa nazalisha mazao ya wastani kwani heki moja ya mahindi nilikuwa napata gunia 3 mpaka 4 lakini kwa sasa kilimo himilivu kinanisaidia kuzalisha maguni 8 hadi 10.

Afisa Kilimo wa kata ya Hombolo Bwawani, Paschal Chuba Sabunyoni anasema uanzishwaji wa mashamba darasa umesaidia wakulima kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kufanya kilimo himilivu.

“Mwanzo wakulima walikuwa wanaeleza kuwa walikuwa hawafahamu kilimo himilivu Lakini kupitia shamba darasa wamejifunza mengi katika uandaaji wa mashamba, utumiaji wa mbolea na maandalizi ya vifaa katika kilimo kulingana na aina ya mazao, pia utumiaji wa mbegu zilizo bora” alisema Sabunyoni.

“Changamoto wakulima wanadai kuwa mvua ni chache kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kusababisha kuwachanganya lakini mashamba darasa yamekuwa na tija kwao kwani wanajifunza mbinu na ujuzi wa kuzalisha mazao yenye tija na kilimo himilivu imekuwa nguzo kuwawezesha wakulima kutumia maji kwa ufanisi na kumsaidia mkulima kutumia mbegu bora na kuondokana na kilimo cha mazoe na imechangia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao na kuondokana na Njaa”

Mradi huu unawasaidiaje wakulima kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi??

Bw,Sigismund Mujuni ni mwakilishi wa Mradi wa kilimo himilivu na afisa kilimo kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (International Institute of Tropical Agriculture -IITA),anasema kwa kushirikiana na serikali wanawajengea uwezo wakulima kuendesha kilimo himilivu kwa ajili ya usalama wa chakula na mradi huu wa serikali ya Tanzania kupita Wizara ya kilimo unatekelezwa katika wilaya 6 za Tanzania bara na wilaya 4 za visiwani Zanzibar ili kuwasaidia wakulima kutambua namna bora ya kukabiliana na changamoto za athari ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunawaelimisha wakulima namna bora ya uvunaji wa maji shambani pamoja na kutumia makinga maji kupitia mashamba darasa lakini pia matumizi ya mbegu bora zinazovumilia ukame ikiwa ili kuwa na uzalishaji wenye tija”
“Wakulima wanatakiwa kutumia mbinu bora za kilimo cha matuta, kilimo cha matuta ya kufunga, na kilimo kinachoitwa ‘Fanya Juu’ Chini’

Majukwaa hayo ya mfano katika kuhimiza kilimo himilivu (Climate Smart Agriculture – CSA) yanalenga kuwapatia taarifa wakulima kuhusu hali ya mabadiliko ya tabianchi, kuleta pamoja washirika, kufanya uratibu wa pamoja juu ya mabadiliko ya tabianchi na kuangalia teknolojia na mbinu zinazofaa kwa ajili ya kufanya kilimo himilivu kulingana na mazingira ya eneo la Mkoa wa Dodoma.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la CARE International Tanzania Bi.Haika Mtui anasema asilimia 65 ya wananchi wanategemea kilimo hivyo wataendelea kushirikiana na serikali ili kuboresha maisha ya wakulima na wananchi.

“kuongezeka ka shughuli nyingi za binadamu zimechangia mabadiliko ya tabianchi ambayo yana madhara mengi, hususani katika kilimo kinachotegemea mvua nchini ambapo uchumi wa Tanzania unategemea kilimo na kilimo kinachangia pato la taifa kwa asilimia 30”

“Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa na athari kubwa na kusababisha kubadilika kwa misimu mvua nyingi kupita wastani na kusababisha mafuriko na kuleta maafa makubwa kwani watu kupoteza maisha miundobinu kuharibika na kurudisha nyuma uchumi wa nchi”

Afisa kilimo Jiji la Dodoma Prakiseda kashaija anasema kilimo himilivu ni kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na mvua kutonyesha kwa wakati na wakati mwingine kunyesha katika mtawanyiko usiostahili hivyo kilimo himilivu kimekuwa mkombozi wa chakula kwa wananchi.

“Wananchi wanauhakika wa chakula na uzalishaji umeongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo mkulima alikuwa anatumia nguvu kubwa na uvunaji wake ni hafifu kwa sasa mkulima anauwezo wa kuvuna Gunia 10 za mahindi kwa Heka 1”

Makala hii imehoji nini kifanyike ili kukabiliana na Mabadiliko ya hali ya hewa ili kuendelea kuzalisha mazao ya kilimo kwa tija.

Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira Seleman Jafo katika kutambua athari za mabadiliko ya tabia Nchini Nchin Tanzania June 4 mwaka huu 2021 alizinduzua  Mpango Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 2021 hadi 2026 .

“Mkakati huo utasaidia kuondokana na uharibifu wa mazingira uliopo kwa sasa kwani athari moja wapo ambayo imetokana na Mabadiliko ya tabianchi na Nchini Tanzania ni maji ya ziwa Tanganyika yameongezeka na kufikià mita mbili Jambo ambalo si salama kwa maisha ya binadamu”

Mabadiliko ya tabia nchi ni suala mtambuka ambalo linahitaji jitihada mbalimbali za wadau na jamii kwa ujumla ili kupunguza viashiria vinavyosababishia kuwepo mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia nishati mbadala ili kupunguza gesi ukaa ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la joto Duniani.