Dodoma FM

Shule Shikizi ya Segu chini kujengwa chumba kimoja cha darasa

13 Aprili 2026, 17:16

Picha ni jengo la Shule Shikizi Segu chini. Picha na Dodomacc

Shule shikizi hiyo itasaidia watoto hasa wa madarasa ya chini wanaoishi maeneo ya mbali kupata elimu karibu, ambapo wanatembea umbali wa km 7 kufika Shule ya Msingi Nala kusoma na wengine kutembea umbali wa km 8 kufika Shule ya Msingi Chihoni kusoma.

Na Mariam Kasawa.

Ujenzi wa Shule Shikizi Segu chini inayosimamiwa na Shule mama ya Msingi Chihoni ulitengewa shilingi 23,000,000 kutoka mapato ya ndani kwaajili ya ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na shilingi 7,200,000 kwaajili ya ujenzi wa matundu manne ya vyoo.

Akiwa katika eneo la mradi, Mhandisi wa miradi wa Kanda Namba Tatu, Mh. Issa Mohamed alikabidhi mchoro wa ramani ya jengo la pili kwaajili ya ujenzi wa darasa moja na kuwahimiza kuanza ujenzi mara moja kwasababu fedha zimeshaingizwa kwenye akaunti ya shule kwaajili ya utekelezaji na wazingatie vigezo na ubora wa ujenzi.

Nae, Afisa Elimu wa Kanda Namba Tatu, Mwl. Robert Tesha aliwaeleza wasimamizi wa mradi ambao ni Shule ya Msingi Chihoni na mkandarasi kutekeleza ujenzi huo kwa weledi na wahakikishe wanafuata taratibu zote za ujenzi ili kupata miundombinu mizuri ya watoto kujifunzia na walimu kufundishia.