Dodoma FM
Dodoma FM
19 March 2026, 16:24

Ufuatiliaji wa biashara unalenga kuhakikisha kila mfanyabiashara anafanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu .
Na Mariam Kasawa.
Watendaji wa Mitaa na Kata kutoka Kanda Namba Mbili aktika Manisipaa ya Dodoma wamekumbushwa kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za ujenzi pamoja na biashara zinazofanyika katika maeneo yao, ili kudhibiti ujenzi holela na kuhakikisha mipango ya miji inatekelezwa kwa mpangilio unaozingatia sheria na kanuni zilizowekwa.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji hao, Meneja wa Kanda Namba Mbili, Abeid Msangi alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kushirikiana kwa karibu katika usimamizi wa maendeleo ya mitaa yao.
Aidha alisisitiza umuhimu wa watendaji hao kuandaa taarifa za mara kwa mara kuhusu zoezi la ufuatiliaji wa ujenzi na biashara. “Ni muhimu mkawa na utaratibu wa kuandaa taarifa za mara kwa mara kuhusu mnachokifanya. Hii itatusaidia kufahamu maeneo yenye changamoto na yale yenye mafanikio, na hivyo kuweka mikakati sahihi ya kuboresha zaidi” alisisitiza Msangi.

Vilevile, aliongezea kwa kusema kuwa ufuatiliaji wa biashara unalenga kuhakikisha kila mfanyabiashara anafanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, na kuhakikisha analipa tozo na kodi zote zinazohitajika na serikali. Hii ni hatua muhimu ya kudumisha nidhamu ya biashara na kuhakikisha ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mtaa wa Chang’ombe, Kata ya Ihumwa, Halima Feruzi, alisema kikao hicho kimekuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.