Dodoma FM
Dodoma FM
18/03/2026, 17:38

Hata hivyo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewataka wananchi na taasisi zote kuhakikisha wanafuata taratibu za mipango miji na kupata vibali stahiki kabla ya kuanza ujenzi, ili kuepusha hasara na migogoro ya kisheria.
Na Anwary Shaban.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa ilani kwa wananchi pamoja na taasisi zote zinazomiliki viwanja ndani ya jiji la Dodoma kuhakikisha wanaviendeleza kwa mujibu wa sheria, huku ikionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe, amesema halmashauri imeamua kutoa taarifa hiyo kwa umma ili kuwahamasisha wamiliki wa viwanja kuviendeleza kulingana na matakwa ya sheria.
Amesema wito huo unatokana na matakwa ya Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999 (Sura ya 113) ambayo inawataka wamiliki wa ardhi kuitumia na kuiendeleza kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa.
Aidha, Gondwe ameongeza kuwa halmashauri itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaofanya maendeleo ya kudumu kama kujenga majengo bila kuwa na vibali halali vya ujenzi.
Amefafanua kuwa hatua hizo ni pamoja na ubomoaji wa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria, akibainisha kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya Mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 8 ya Mwaka 1982, ambazo zinaelekeza wazi kuwa kila jengo linalojengwa ndani ya mamlaka ya mji au jiji lazima liwe na kibali cha ujenzi.