Dodoma FM
Dodoma FM
02/03/2026, 18:09

Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msisitizo katika usimamizi madhubuti wa fedha za umma, kukamilisha miradi ya maendeleo na kuimarisha miundombinu ya jiji, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma na kuchochea maendeleo ya wananchi wa Dodoma.
Na Anwary Shaban.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limefanya kikao maalum kujadili na kutoa mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo mkoani Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mchumi wa Jiji la Dodoma, Francis Kaunda, amesema kuwa bajeti ya mwaka 2026/2027 itaweka mkazo zaidi katika miradi ya maendeleo pamoja na kuhakikisha miradi yote inayoendelea inakamilika kwa wakati. Amesisitiza kuwa lengo la halmashauri kwa kushirikiana na Serikali ni kuona fedha zinazotengwa zinaleta tija kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha, Kaunda ameeleza kuwa halmashauri imejipanga kuhakikisha stahiki za madiwani, watumishi pamoja na gharama za uendeshaji wa ofisi zinalipwa kwa wakati. Ameongeza kuwa bima za magari na majengo zinaendelea kulipwa kama inavyotakiwa, sambamba na mpango wa ununuzi wa magari mapya kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Federick Segamiko, amewashukuru madiwani kwa ushirikiano wao mkubwa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, akibainisha kuwa hali ya utekelezaji wa miradi kwa sasa ni ya kuridhisha na miradi mingi inaendelea kusonga mbele kama ilivyopangwa.
Sanjari na hayo, Dkt. Segamiko amebainisha kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti za miradi ya upimaji shirikishi, na kwamba moja ya maelekezo yatakayotolewa ni kuelekeza fedha hizo katika kufungua barabara ili kuboresha miundombinu na kurahisisha huduma kwa wananchi.