Dodoma FM
Dodoma FM
10 February 2026, 10:37 am

Kwa Tanzania na nchi nyingine zinazokabiliwa na ukame, uwekezaji katika mbegu himilivu na kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi si hiari tena—ni hitaji la dharura.
Na Mariam Kasawa.
Katika miaka ya karibuni, mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuitikisa dunia, yakiacha athari kubwa katika sekta ya kilimo.
Ukame wa mara kwa mara, misimu isiyotabirika ya mvua na ongezeko la joto, vimewaacha wakulima wadogo katika hatari ya njaa na umasikini.
Ndiyo maana katika mikutano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo COP30, matumizi ya mbegu himilivu yamepewa kipaumbele kama suluhisho la kuokoa kilimo na kuhakikisha uhakika wa chakula.
Lakini kwa Tanzania, mjadala huu haukubaki kwenye majukwaa ya kimataifa pekee.
Ndani ya Bunge la 13 jijini Dodoma, wabunge waliibua kwa kina suala la mbegu himilivu, wakisisitiza umuhimu wake katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko, alihoji mkakati wa Serikali katika kuongeza upatikanaji wa mbegu za muda mfupi, hususan kipindi cha masika, ili kuwaepusha wakulima na hatari ya njaa.
Swali lake liliakisi kilio cha wakulima wengi wanaokabiliwa na misimu mifupi ya mvua na ukame wa mara kwa mara.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, alisema wizara yake inaendelea kufanya tathmini ya mwenendo wa mvua na hali ya hewa, huku ikiandaa mbegu za muda mfupi na muda mrefu, sambamba na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Kwa mujibu wa Serikali, mkakati huo unalenga kuwawezesha wakulima kuendelea kuzalisha hata katika mazingira yasiyotabirika ya tabianchi.
Hata hivyo, bado maswali yanaendelea kuibuka, hasa kwa wakulima wa mikoa inayokabiliwa na ukame kama Dodoma.
Wanauliza—mbegu hizi zinasambazwa lini? Zinamfikia mkulima wa mwisho? Na je, zinatosha mahitaji halisi?
Katika mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Dira ya Taifa ya 2050, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, alihoji kwa nini taasisi kama Wakala wa Mbegu za Kilimo,( ASA), na wazalishaji binafsi wa mbegu himilivu zisiwezeshwe zaidi kwa miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Makete, Festo Sanga, alisema sekta ya kilimo ndiyo inayoathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, na akaisisitiza Serikali kuwekeza kwa nguvu katika kilimo cha umwagiliaji.
Katika ngazi ya kimataifa, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, katika mkutano wa COP30 uliofanyika Belém, Brazil, lilipendekeza matumizi ya mbegu himilivu likieleza kuwa zina uwezo wa kustahimili ukame na misimu isiyotabirika ya mvua.
FAO linaeleza kuwa mbegu himilivu ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha familia na jamii zinapata chakula cha kutosha.
Hata hivyo, shirika hilo linaonya—bila usambazaji kwa wakati, uwekezaji wa kutosha na ufuatiliaji madhubuti, mikakati hiyo hubaki kuwa sera na kauli zisizoleta matokeo kwa wananchi.
Hatua hizi zinaweza kuwa nguzo ya kuokoa maisha, kuimarisha uhakika wa chakula na kujenga mustakabali wa kilimo endelevu kwa vizazi vijavyo.