Dodoma FM

‘Kushiriki shughuli za maendeleo ni wajibu kwa mwananchi’

14 January 2026, 2:50 pm

Picha ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini Mhe. Anthony Mavunde akiwa na baadhi ya wananchi wa Nkulabi, kata ya Mpunguzi jijini Dodoma katika ujenzi wa shule ya sekondari Nkulabi. Picha na Dodoma City Council.

Sheria ya Serikali za Mitaa Sura ya 287 ( Mamlaka za Serikali za Mitaa- Wilaya) na Sura ya 288 ( Mamlaka za Serikali Mitaa- Miji) zinatambua na kusisitiza wananchi katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, kuhudhuria mikutano ya vijiji au mtaa pamoja na kuchangia nguvu kazi.

Na Lilian Leopold.

Imeelezwa kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki na kushirikishwa kikamilifu katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa  katika mtaa wake, ikiwemo ujenzi wa shule, barabara pamoja na suala la ulinzi na usalama ili kujenga mtaa wenye maendeleo endelevu na manufaa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 27 kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Hayo yamebainishwa na Issa Rashis, Mjumbe wa kamati ya serikali ya mtaa wa Mathias kata ya Miyuji, jijini Dodoma akimwakilisha Mwenyekiti wa mtaa huo, amesema ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na inaleta tija kwa jamii.

Ameeleza kuwa wananchi wa mtaa wa Mathias wamekuwa mstari wa mbele kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa kutoa nguvu kazi, pamoja na ushauri .

Sauti ya Issa Rashid.

Aidha, Issa ameongeza kuwa serikali ya mtaa huo inaendelea kuhakikisha kunakuwepo na uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika hatua zote za maamuzi ya miradi ya maendeleo, hali inayowezesha wananchi kutambua, kufuatilia na kuelewa miradi katika mtaa wao.

Sauti ya Issa Rashid.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa mtaa huo wamesema wanashiriki katika shughuli za kimaendeleo kwa kutoa nguvu kazi  pamoja na kuchangia mawazo yanayolenga kuboresha maendeleo ya eneo lao.

Sauti za wananchi.

Akihitimisha, Issa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya mtaa ili kuwasilisha changamoto na mapendekezo yao, hatua itakayosaidia uongozi kuzifanyia kazi kwa wakati na kuimarisha maendeleo ya mtaa.