Watendaji wa serikali watakiwa kutatua kero za wananchi
25 October 2023, 1:02 pm
Katika Mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Bahi Mh Godwin Gondwe aliambatana na kamati ya usalama ya wilaya hiyo.
Na Bernad Magawa
Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwa amewaagiza watendaji wa Serikali katika ngazi zote wilayani humo kuhakikisha wanasikiliza na kutatua kero zao kikamilifu huku akisema kuwa hatua kali za kiutumishi zitachukuliwa kwa wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.
Mheshimiwa Gondwe ameyasema hayo kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Bahi Sokoni eneo la Mwanachugu kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi huku akiambatana na kamati ya usalama ya wilaya hiyo, wakuu wa Idara pamoja na wakuu wa taasisi za serikali na kuongeza kuwa wilaya imetenga siku ya Alhamisi kuwa siku maalumu ya kusikiliza kero za wananchi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bahi Zaina Mlawa amewaagiza viongonzi wa serikali za vijiji kuhakikisha wanasoma mapato na matumizi kwenye mikutano ya hadhara huku akiwasihi wananchi kuendelea kuwatumia vongozi wao katika kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.
Awali, Wananchi waliokusanyika katika mkutano huo walipata nafasi ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili ambapo pamoja na mambo mengine bado suala la kukosekana kwa soko wilayani hapo likiendelea kuwa kero kwa wafanyabiashara na kusema kuwa linaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa Bahi.