Wazazi wachangia kuchelewesha upatikanaji haki vitendo vya ukatili dhidi ya watoto
28 May 2021, 1:04 pm
Na; Mariam Matundu.
Baadhi ya Wazazi na walezi Mkoani Rukwa wameelezwa kuchangia kuchelewesha upatikanaji wa haki kwa waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Akizungumza na wadau wa Jukwaa la Haki Jinai Mkoani Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka Maafisa Ustawi wa Maendeleo ya Jamii kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuhakikisha jamii inabadili mitazamo na kushiriki katika mchakato wa kupatikana haki kwenye kesi za ukatili kwa watoto.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa Maafisa Ustawi na Maendeleo wa Jamii wana jukumu la kubadili fikra za jamii ione umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya Serikali katika kushughulikia mashauri ya Ukatili dhidi ya watoto na kwamba masuala haya ni makubwa na yanaacha makovu makubwa kwa watoto.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome, akizungumza katika kikao hicho amewataka watendaji wote wanaohusika katika mchakato wa utoaji haki, kufuata Sheria, kanuni na taratibu na kufanya kazi kwa weledi ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Mpango wa Kitaifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Faustina Vallery amesema changamoto zilizopo ni pamoja na kukosa mahabusu za watoto pamoja na uhaba wa watumishi japokuwa wanapata ushirikiano na mamlaka nyingine Mkoani hapo.
Ziara ya Makatibu Wakuu hao inafanyika kwa lengo la kujadili na watendaji na kuona namna ya kutatua changamoto za masuala yanayozigusa Wizara hizo kwa pamoja hususani suala la kushughulikia mfumo wa haki za makosa ya jinai kama ya ukatili dhidi ya watoto.