Dodoma FM
Dodoma FM
2 April 2026, 16:50

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Hospitali ya Mirembe, Dodoma, yakiwa na lengo la kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu hali ya usonji pamoja na kuboresha mazingira kwa watu wenye usonji. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Weka Tumaini Usoni Mwao, Furahia Utofauti.”
Na Benard Komba.
Hospitali ya Afya ya Akili ya Taifa Mirembe imetakiwa kuimarisha usimamizi shirikishi kwa kushirikiana na taasisi binafsi ili kuwezesha tathmini ya watoto wenye usonji kufanyika kila robo mwaka.
Hayo yameelezwa na Dkt. Omary Ubuguyu, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma.
Dkt. Ubuguyu ameipongeza hospitali hiyo kwa juhudi zake za kutoa huduma kwa watoto wenye changamoto ya usonji, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na taasisi binafsi, ikiwemo shule maalum, ili kuboresha zaidi huduma kwa jamii.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Maalum wa Jiji la Dodoma, Issa Omary Kambi, amesema halmashauri inaendelea kuwatambua watoto wenye usonji ili kuwaingiza katika mfumo wa bima ya afya kwa wote, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Afya ya Akili ya Taifa Mirembe, Dkt. Godwin Mwisomba, amesema hospitali hiyo inaendelea kushirikiana kwa karibu na jamii ili kuonesha upendo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ya akili.