Dodoma FM
Dodoma FM
16/03/2026, 17:19

Wananchi wameiomba serikali kuharakisha kuchukua hatua za kudumu ili kuhakikisha usalama wa watoto na wakazi wa Kaloleni.
Na Kitana Hamis.
Wananchi wa Kata ya Kaloleni wilayani Kiteto mkoani Manyara wamelalamikia uwepo wa korongo kubwa linalokatiza eneo lao, wakisema linahatarisha usalama wa watoto na wakazi hasa wakati wa mvua.
Wananchi hao wamesema kuwa mvua zinaponyesha maji hujaa kwenye korongo hilo na kufanya njia ishindwe kupitika, hali inayowafanya watoto kushindwa kwenda shule na wengine kuchelewa kufika mashuleni.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wameiomba serikali kuharakisha kuchukua hatua za kudumu ili kuhakikisha usalama wa watoto na wakazi wa Kaloleni unalindwa.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa eneo hilo amesema tatizo la korongo hilo limekuwepo kwa muda mrefu na limekuwa likiwaathiri wakazi wengi, hususan wanafunzi wanaokwenda shule kila siku.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilayani Kiteto, Magiri, amesema tayari wameanza kuchukua hatua za muda mfupi za kudhibiti maji ili kupunguza hatari inayosababishwa na korongo hilo, huku wakipanga kuboresha miundombinu ya kudumu katika eneo hilo.