Dodoma FM
Dodoma FM
16/03/2026, 13:43

Meneja wa Kitengo cha Majitaka na Usafi wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Ores John, amesema kuwa mamlaka hiyo inashirikiana na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha matengenezo yanafanyika haraka.
Na Anwary Shaban
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeanza mara moja kushughulikia changamoto iliyojitokeza kufuatia kubomoka kwa bomba kubwa la majitaka lenye kipenyo cha milimita 760 katikati ya barabara inayounganisha mikoa ya Singida na Dar es Salaam, katika eneo la Chako ni Chako jijini Dodoma.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Meneja wa Kitengo cha Majitaka na Usafi wa Mazingira DUWASA, Mhandisi Orest John, amesema mamlaka hiyo imeanza hatua za haraka za ukarabati kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kurejesha huduma ya usafiri katika barabara hiyo muhimu kwa haraka iwezekanavyo.

Mhandisi John ameeleza kuwa tayari maandalizi yote muhimu yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kupeleka mitambo na vifaa vya kazi katika eneo la tukio, na kwamba kazi ya ukarabati imeanza rasmi. Amesema lengo ni kuhakikisha barabara hiyo inarejea katika hali yake ya kawaida mapema ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku bila usumbufu.
Kwa mujibu wa Mhandisi huyo, iwapo hakutajitokeza changamoto nyingine zaidi ya zilizopo sasa, matengenezo ya bomba hilo yanatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha siku saba.
Wakati huohuo, baadhi ya wananchi wa Dodoma wameiomba Serikali kuharakisha kukamilisha na kufungua barabara ya mzunguko ya nje ya Jiji la Dodoma. Wamesema hatua hiyo itasaidia magari makubwa ya mizigo kupita nje ya jiji, hivyo kupunguza msongamano wa magari na adha ya usafiri katika maeneo ya katikati ya jiji.