Dodoma FM
Dodoma FM
26/02/2026, 12:10

Mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za pamoja za serikali na wadau kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya elimu bora ya awali na kuandaliwa kuwa wananchi wenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Na Farashuu Abdallah.
Katika juhudi za uboreshaji na utiaji nguvu wa Elimu ya awali kuanzia watoto wenye umri wa miaka 5-6 kwa lengo la kuboresha KKK yaani kusoma,kuandika na kuhesabu wadau mbalimbali wameonesha jitihada katika hili na kueleza mafanikio yaliyopatikana.
Akizungumza leo meneja miradi ya CIC mkoa wa Dodoma Bw.Faraji Paragha katika mkutano wa program ya Elimu ya awali Dodoma ukumbi wa Hotel ya Royal Village amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika mradi huu ni pamoja na kutoa elimu ya kuwajengea uwezo walimu wa awali, maafisa elimu na kushirikisha wazazi katika kusimamia ubora wa maendeleo ya watoto shuleni.
Aidha ameongeza kuwa katika mradi wa CIC wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya watoto kujifunzia.
Nae mkurugenzi wa wa Children in Crossfire (CiC), Craig Ferla, amesema mustakabali wa Tanzania uko mikononi mwa watoto wa sasa na vizazi vinavyokuja, akisisitiza umuhimu wa kuelekeza nguvu zote katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Akitoa wasilisho wakati wa ufunguzi wa mkutano wa programu ya elimu ya awali uliofanyika jijini Dodoma, Ferla amesema pamoja na kizazi cha Gen Z kinachoonekana kwa sasa, kuna vizazi vingine kama kizazi Alpha, Beta na Gamma vinavyokuja ambavyo ni hazina muhimu ya Taifa siku za usoni.

Alisema Tanzania imejizatiti katika kuimarisha maendeleo ya watoto kupitia mikakati ya kisayansi ikiwemo mpango wa kujenga umahiri wa K tatu na Dira ya Taifa ya 2050 inayolenga ukuaji wa ubongo wa mtoto na kufikia utimilifu wao, huku akibainisha kuwa watoto wa awali ni msingi wa kujenga rasilimali watu wenye tija hapo baadaye.
Naye Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Kiduma Mageni, alisema kupitia ushirikiano na Children in Crossfire, mkoa umefanikiwa kujengewa madarasa mapya 33 na kukarabati madarasa ya awali 473, hatua iliyobooresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hususan katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Aidha, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shule za Msingi, Ephram Simbeye, alipongeza jitihada za shirika hilo katika kuunga mkono juhudi za serikali kuimarisha sekta ya elimu na kuendeleza agenda ya maendeleo ya mtoto nchini.