Dodoma FM
Dodoma FM
20 February 2026, 5:41 pm

Kiwanja hicho kinajengwa katika ‘Package 2’ ambapo ‘Package 1’ inatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 165.627 bila VAT na ‘Package 2’ inatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 194.403 bila VAT.
Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato wametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mradi kutoka kwa wahandisi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa serikali ina matarajio makubwa na uwanja huo, akisisitiza kuwa ni mradi wa kimkakati utakaosaidia kukuza uchumi wa mji mkuu na maeneo jirani. “Nimeridhishwa na maendeleo ya mradi huu na ubora wa kazi unaoendelea, kasi iongezeke ili malengo ya ukamilishaji yatimie kama ilivyopangwa” alisema Shekimweri.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Miradi ya Maendeleo Mkoa wa Dodoma kutoka TANROADS, Mhandisi Colman Ramadhani alisema kuwa ujenzi wa miundombunu ya uwanja umefikia asilimia 83 huku ujenzi wa majengo mengine umefikia asilimia 67.
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kinatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vya ndege vya kisasa nchini Tanzania, ukiwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za kimataifa na kuongeza fursa za biashara, usafirishaji na utalii.