Dodoma FM

Senyamule asisitiza umuhimu wa lishe kwa watoto

18 February 2026, 4:02 pm

Picha ni kikao cha kwanza cha ajenda ya lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichowakutanisha wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa.Picha na Anwari Shaban.

Kwa mujibu wa takwimu za kikao hicho, mkoa wa Dodoma umeendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za lishe, huku juhudi zaidi zikielekezwa katika kuongeza uelewa wa jamii na kuboresha huduma kwa watoto wa shule za msingi na sekondari.

Na Anwary Shaban.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh.Rosemary Senyamule, amesisitiza umuhimu wa lishe bora kwa watoto, akieleza kuwa mabadiliko makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa afua za lishe ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mheshimiwa Senyamule ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kwanza cha ajenda ya lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichowakutanisha wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa, kilichofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho, amesema Serikali inatambua umuhimu wa lishe bora kwa watoto na imeweka mikakati madhubuti ikiwemo mikataba ya utendaji kazi kwa Wakuu wa Mikoa ili kuhakikisha wanafunzi wanapatiwa lishe bora shuleni.

Sauti ya Mh. Rosemery Senyamule

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mwanahamisi Ally, amesema kikao hicho kimejadili maendeleo ya utekelezaji wa afua za lishe katika mkoa wa Dodoma pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza.

Picha ni kikao cha kwanza cha ajenda ya lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichowakutanisha wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa.Picha na Anwari Shaban.

Ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto hizo ni uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu umuhimu wa lishe bora, hali inayochangia kuwepo kwa udumavu na matatizo mengine ya kiafya kwa watoto.

Sauti Mwanahamisi Ally,

Naye Afisa Lishe wa Jiji la Dodoma,Bi. Semenieva Juma, amesema kuwa kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2025, wamefanikiwa kuwafikia watoto kwa asilimia 91 katika utekelezaji wa huduma za lishe.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya wataalamu wa afya, viongozi wa serikali za mitaa pamoja na kampeni za uhamasishaji kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora.

Bi. Semenieva Juma.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameagiza watumishi wa umma kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na kusimamia ipasavyo sekta ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanarudi na kubaki shuleni.

Sauti ya Mh. Rosemery Senyamule