Dodoma FM
Dodoma FM
16 February 2026, 3:50 pm

Kupitia kongamano hilo, Kata ya Zuzu inatarajia kuona kizazi cha vijana chenye mwamko mpya wa uzalendo, uwajibikaji na uthubutu wa kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Na Anwary Shaban.
Zaidi ya vijana 600 wa Kata ya Zuzu, jijini Dodoma, wanatarajia kunufaika na mafunzo waliyo yapata kupitia Kongamano la Vijana lililoandaliwa kwa lengo la kuwawezesha vijana kielimu, kiuchumi na kijamii.
Kongamano hilo limefanyika katika Kata ya Zuzu, likiwakutanisha vijana kutoka mitaa mbalimbali kwa lengo la kujadili fursa zilizopo na namna ya kuzitumia kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Tarafa ya Zuzu, Ibrahim Hassan, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaj Jabir Shekimweri, aliwahimiza vijana kuacha dhana potofu kuwa hakuna fursa katika maeneo yao na badala yake wajikite katika kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa Taifa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Zuzu, Mhe. Jenesta Malingo, amesema wazo la kuandaa kongamano hilo limetokana na kutambua changamoto zinazowakabili vijana, hususan ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo.
Sambamba na hilo, Mrakimu Msaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, ASP Crista Kayombo, ametoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na kuwasihi wananchi kushiriki katika nyumba za ibada kama njia mojawapo ya kuimarisha maadili na kupunguza vitendo vya ukatili katika jamii.
Naye mmoja wa vijana walioshiriki kongamano hilo, Enyasi Lazaro, amesema elimu waliyoipata imewafumbua macho kuhusu athari za dawa za kulevya, umuhimu wa kutunza fedha na kuchangamkia fursa zilizopo badala ya kubweteka vijiweni wakisubiri ajira.