Dodoma FM

ITU yaitaja Tanzania kuwa kinara usalama mtandaoni

10 February 2026, 5:05 pm

Tanzania inashika nafasi ya 45 duniani kwa viwango vya usalama wa mitandao.Picha na Anwary Shaban.

Maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni yanaendelea kutumika kama jukwaa muhimu la kuelimisha jamii juu ya matumizi salama ya teknolojia ya habari, huku Tanzania ikiendelea kuimarisha nafasi yake katika usimamizi wa usalama wa mtandao kikanda na kimataifa.

Na Anwary Shaban.
Tanzania imetajwa na Shirika la Mawasiliano Duniani ITU kupitia kitengo chake cha usalama mtandaoni kuwa kinara katika viwango vya usimamizi wa usalama mtandaoni kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku ikishika nafasi ya 45 duniani kwa viwango vya usalama wa mitandao.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Nicholus Mkapa, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mgeni Rasmi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Kairuki, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni. Mkapa amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za serikali katika kuimarisha mifumo ya usalama wa kimitandao na sera zinazolenga kulinda watumiaji wa mtandao.

INSERT………………………………………………NICHOLUS MKAPA

Aidha, Nicholus Mkapa amesisitiza umuhimu wa kuwaelimisha watoto kuhusu matumizi salama ya mtandao, akisema elimu hiyo itawasaidia kujilinda dhidi ya hatari za mtandaoni na kutumia teknolojia kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla. Ameongeza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wananchi wote wanatumia mtandao kwa usalama.

Kwa upande wake, Mwalinde Kato kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu amesema endapo watoto hawatatumiwa mtandao kwa kuzingatia umri na maadili, wanaweza kuingia au kufanyiwa vitendo vya ukatili. Amesema maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni yanalenga kuongeza uelewa kwa jamii juu ya hatari hizo na namna ya kujikinga

Naye mwanafunzi Anna Komba amesema mafunzo waliyoyapata yamewasaidia kufahamu matumizi bora ya mitandao ya kijamii, akisema sasa wanajifunza kuitumia mitandao kwa ajili ya elimu, kujifunza na maendeleo, huku wakiepuka matumizi yasiyo sahihi.

Sauti ya kina