Dodoma FM
Dodoma FM
05/02/2026, 16:27

Uzinduzi wa mradi wa Tuinuke Pamoja unalenga kukuza uchumi wa wanavikundi mbalimbali ikiwemo makundi maalumu, huku serikali ikiahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwaunga mkono wananchi kupitia vikundi vilivyojisajili, ikiwemo vikundi 57 ambavyo tayari vimesajiliwa hadi sasa wilayani Kondoa.
Na Mariam Matundu.
Taasisi ya Agha Khan Foundation imefanya uzinduzi rasmi wa mradi wa Tuinuke Pamoja uliofanyika wilayani Kondoa mkoani Dodoma, mradi unaolenga kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake, wanaume pamoja na makundi maalumu, sambamba na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jamii.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu, ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, Bi Felista Mdemu, ametoa rai kwa viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanawabaini na kuwawezesha wanawake wenye ulemavu pamoja na makundi maalumu ili kuimarisha usawa wa kijinsia katika jamii.
Aidha, Bi Mdemu ameongeza kuwa ni wakati sasa kwa wanawake wa Kondoa kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa kutoa elimu hiyo katika mikoa mingine, ili jamii pana iweze kunufaika na kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wao, Nicola Brennankutoka Ubalozi wa Ireland nchini Tanzaniapamoja na Atteya Sumar, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Aga Khan Foundation, wameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika utekelezaji wa mradi wa Tuinuke Pamoja, wakisema serikali imekuwa chanzo kikubwa cha msaada katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Naye Nestory Muhando, ambaye ni Meneja wa Mradi wa Tuinuke Pamoja, amesema mradi huo unafanya kazi kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii vilivyojikusanya kwa hiari kwa ajili ya kutatua changamoto zao, vikundi ambavyo vimetambuliwa rasmi na halmashauri, huku wengi wa wanavikundi hao wakiwa ni wanawake.