Dodoma FM
Dodoma FM
30 January 2026, 5:19 pm

Zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji cha Mbuyuni ni sehemu ya mkakati wa pamoja kati ya serikali na DUWASA wa kulinda mazingira nakuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Wilaya ya Kongwa.
Na Anwary Shaban.
Wakulima walio vamia eneo la chanzo cha maji Mbuyuni Wilayani Kongwa na kufanya shughuli za kilimo na ujenzi wa nyumba wametakiwa kuondoka katika eneo hilo mara moja.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandajimiti lililofanyika katika chanzo hicho cha maji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa matumizi ya sasa na ya baadae.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Mhe. Simon amesema kuwa chanzo chamaji hakina siasa, na kusisitiza kuwa serikali haitasita kuwakamata nakuwafikisha mahakamani wananchi wote watakaobainika kulima, kujenga au kuharibu mazingira katika eneo hilo kinyume na sheria.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Eng. Aron Joseph, Mtendaji wa DUWASA, Rahel Muhando, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutambua mchangomkubwa wa mazingira katika uhifadhi na uendelevu wa vyanzo vya maji.
Rahel amesisitiza kuwa upandaji miti ni njia mojawapo muhimu ya kulinda vyanzo vya maji ili viendelee kutoa huduma kwa muda mrefu kwa wananchi wa Kibaigwa na maeneo jirani.
Nao baadhi ya wakulima na wananchi wa eneo hilo wameeleza kuwa uharibifu wa vyanzo vya maji unaotokana na shughuli za kibinadamu umeleta athari mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mazingira, kupungua kwa maji, pamoja na kuharibika kwa miundombinu ya maji.
Wananchi hao wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji ili kuepusha madhara zaidi.