Dodoma FM
Dodoma FM
23 September 2025, 3:45 pm

Amewaomba wafanyabiashara kutumia fursa ya zoezi hilo la elimu ya kodi mlango kwa mlango kwa ajili ya kutoa changamoto zao za kikodi zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Na Lilian Leopold.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma Bw. Pendolake Elinisafi, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi ya awamu ya tatu kwa wakati kabla ya tarehe 30.09.2025 ili kuepuka faini zisizo za lazima.
Akizungumza wakati wa zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango linalofanyika mkoani humo, Meneja huyo ameeleza kwamba, kodi zikilipwa mapema zitasaidia serikali kutekeleza mipango ya maendeleo kwa wakati.
Kwa upande wao Wafanyabiashara waliotembelewa katika zoezi hilo, wameipongeza TRA kwa kuja na kampeni hiyo huku wakiziomba Mamlaka nyingine za serikali kuiga mfano wa TRA ili kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Kampeni hiyo ya elimu ya kodi mlango kwa mlango imeanza leo mkoani Dodoma na itamalizika tarehe 1 Oktoba, 2025 ikiwa na lengo la kuwaelimisha walipakodi, kuwatambua walipakodi wapya na kuwasajili sambamba na kusikiliza maoni, ushauri na changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabili ili kuzitatua kwa haraka.