Dodoma FM
Dodoma FM
22 August 2025, 12:41 pm

Picha ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Biteko akitoa maagizo kwa mkandarasi. Picha na Seleman Kodima.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi za
kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai
ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki
kwani wananchi hao wana haki na lazima walipwe fidia.
Na Seleman Kodima.
Kutokana na kusuasua kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka
Chalinze hadi Zuzu Dodoma,Naibu Waziri Mkuu Dkt. Dotto Biteko amemuagiza mkandarasi kampuni
ya TBEA ya China anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa wa
asilimia Saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake
nchini.
Hayo ameyasema wakati akikagua mradi huo katika Kijiji Cha Manchali wilayani Chamwino ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Biteko amekagua
mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka
Chalinze hadi Zuzu Dodoma na kueleza kutoridhishwa kwake na
utekelezaji wa mradi huo ambao ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31
lakini kwa sasa umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba
mwaka 2024.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, sababu zilizotolewa na Mkandarasi za
kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai
ya fidia na kukutana na miamba katika mkuza wa mradi hazikubaliki
kwani wananchi hao wana haki na lazima walipwe fidia.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.
Amesisitiza kuwa njia mpya ya umeme ya kV 400 ni muhimu kwani katika
Mkoa wa Dodoma mahitaji ya umeme yanaongezka kila siku huku mkoa huo
pia ukiwa ni kitovu cha usambazaji umeme katika mikoa yote ya
Magharibi ikiwemo Singida, Tabora, Shinyanga Mara na Kigoma ambayo
inategemea utulivu wa umeme katika Mkoa wa huo na kwamba Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan alishaagiza kuwa mradi huo usichezewe hivyo
Mkandarasi ahakikishe kuwa anaupa umakini mkubwa.
Kutokana na mradi huo kuwa nyuma katika utekelezaji, Dkt. Biteko
amemuagiza Mkandarasi kuja na mpango mpya wa utekelezaji wa kazi
ukiwemo wa kufidia muda uliopotezwa ambapo ametoa siku nne mpango wa
fidia ya muda uwasilishwe kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa Wananchi kutozuia
utekelezaji wa miradi pale inapopita kwenye maeneo yao na Serikali kwa
upande wake itahakikisha kuwa wanapata haki wanazostahili kwani Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza kuwa hataki wananchi wafanyiwe
dhuluma ambapo wasaidizi wake wanahakikisha kuwa agizo hilo
linatekelezwa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa
TANESCO, Lazaro Twange amesema Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa
msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma unakusudia
kusafirisha umeme wote unaozalishwa kutoka katika Bwawa la kuzalisha
umeme la Julius Nyerere (Megawati 2,115) na kuingiza kwenye gridi ya
Taifa kisha kuufikisha kwenye maeneo yote yenye mahitaji ya umeme.
Ameeleza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati yatafanyiwa kazi ikiwemo ya kuhakikisha kuwa mradi
unakamilika mwezi Juni au kabla ya Juni 2026 kwa mujibu wa mkataba.