Dodoma FM
Dodoma FM
31 July 2025, 5:13 pm

Maonesho hayo yamebebwa na Kauli mbiu ya “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.
Na; Mariam Kasawa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amesema kuwa washiriki wapatao 1163 wamethibitisha kushiriki katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane 2025 ambayo Kitaifa yanafanyika katika Viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.
Maonesho ya Nanenane 2025 yanafanyika pia katika kanda saba 7 nchi nzima ambapo yatahusisha washiriki mbalimbali wakiwemo wakulima, waongezaji thamani ambao ni Viwanda, wafanyabiashara; vile vile watafiti, washirika wa maendeleo; taasisi za fedha, kampuni mbalimbali za pembejeo na zana za kilimo na wale wanaohusika na usindikaji, ufungashaji na usafirishaji.

Katika tukio lingine, Katibu Mkuu Mweli amepokea hundi yenye thamani ya shilingi millioni 50 iliyotolewa kwa udhamini wa maonesho hayo kutoka Benki ya CRDB. Ameipongeza Benki hiyo kwa kuwa mdau muhimu wa kuchangia maendeleo katika Sekta ya Kilimo.
Wageni rasmi katika Maonesho ni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 8 Agosti 2025 katika kusherehekea Siku ya Nanenane; ambapo ufunguzi wake wa tarehe 1 Agosti 2025 mgeni rasmi ni Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.