NHIF yarejesha toto afya kadi
18 December 2024, 3:15 pm
Mpango wa Toto Afya Kadi utasaidia familia za wananchi hasa zile zenye watoto wenye changamoto za kiafya.
Na Mariam Matundu.
Waziri wa Afya Mh. Jenista Mhagama amesema kurejeshwa kwa Toto Afya Kadi kutaleta matumaini mapya na uelekeo thabiti wa Bima ya Afya hususan kwa kundi la watoto ambalo linahitaji uangalizi wa pekee.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo Dec 17, 2024 Jijini Dodoma, wakati akizindua vifurushi vitatu vya vya Bima ya Afya kikiwepo cha Toto Afya Kadi.
Waziri Mhagama amesema Mpango huo wa Toto Afya Kadi utasaidia familia za wananchi hasa zile zenye watoto wenye changamoto za kiafya.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa mpango wa sasa wa usajili wa Toto Afya Kadi utafanyika pia kwa mtoto mmoja mmoja iwapo itatokea mtoto husika hayupo shule, hii ni hatua kubwa na yakujivunia katika sekta nzima ya afya.
Mbali na kifurushi cha Toto Afya Kadi kilichozinduliwa , vifurushi vingine ni Ngorongoro chenye huduma 445 na Serengeti chenye huduma 1,815 ambavyo vyote vimelenga kuhudumia watanzania.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dkt. Irene Isaka amesema kuzinduliwa kwa mfumo wa kidijitali kumewawezesha kushughulikia folio 1200 kwa dakika 45 tofauti na awali ambapo walishighulikia folio 800 tu kwa siku.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini Bw. Edga Gabriel amesema kuzinduliwa kutasaidia kutambua viashiria vya awali vya udanganyifu.
Serikali kupitia NHIF imefanikiwa kutengeneza mifumo ya kidijitali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.45 kwa kutumia wataalam wa ndani na kuokoa zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 endapo wangetumia wataalam kutoka nje ya nchi.