Dodoma FM

Muuguzi anayependwa na wananchi wake

2 August 2024, 5:09 pm

Wananchi wa kijiji cha Ngomai wilayani Kongwa wakiwa katika mkutano .Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Harambee hiyo imefanyika wiki hii kijijini hapo ambapo wananchi hao wameweza kuchanga fedha zaidi ya shilingi milioni nne kwa ajili ya kumnunulia kiwanja muuguzi huyo ili aweze kujenga na kuishi kijijini hapo hata atakapostaafu kazini.

Na Bernadetha Mwakilabi.
Wananchi wa kijiji cha Ngomai kata ya Ngomai wilayani Kongwa wamefanya harambee kubwa ya kumpongeza muuguzi wa kijiji chao Bwana Peter Mwakalosi kwa kufanya kazi kwa moyo wa ukarimu upendo kujitoa na kuzingatia maadili ya taaluma yake.

Aidha katika risala yao wananchi hao wamempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na watumishi wenye kujitoa katika jamii akiwemo muuguzi huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia watu wa kijiji hicho na vijiji jirani.

Risala wananchi.

Nae mgeni rasmi katika harambee hiyo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kongwa Dr Omary Nkullo amewapongeza wananchi wa Ngomai kwa kuandaa harambee hiyo wameonesha moyo wa shukrani na jambo la kuigwa kwa watu wengine na kuongeza kuwa hilo ni deni ambalo anatakiwa kulilipa kwa kuipandisha zahanati ya kijiji hicho kuwa kituo cha afya.

Dkt Nkullo amefafanua kuwa harambee iliyofanywa na wananchi hao imeonesha kuwa muuguzi Mwakalosi anatambua nafasi yake katika utendaji wa kazi yake na hii inatokana na kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais dokta Samia ya kulipa watumishi kwa wakati na kuboresha miundombinu ya afya nchini.

Sauti Dkt. Nkullo.
Picha ni kushoto muuguzi aliyepongezwa Bw Peter Mwakalosi, mwenyekiti wa kijiji Cha Ngomai Sospeter Njamas, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kongwa Dkt Omary Nkullo, Diwani kata ya Ngomai Mh Mfaume Mlimila na Mganga mkuu wa wilaya Kongwa Dkt Thomas Mchomvu katika sherehe za kumpongeza muuguzi huyo. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Mfalme Mlimila amemuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kongwa asimhamishe muuguzi huyo kijijini hapo kwani anafanya kazi kubwa ya kutoa huduma nzuri ya afya na wananchi wanamkubali.

Vilevile Mlimila ameongeza kuwa muuguzi huyo alipofika kijijini hapo mwaka 2005 amefanikiwa kuondoa dhana potofu ya wananchi kutibiwa kwa waganga wa kienyeji magonjwa ambayo awali hawakuamini kama yanaweza kutibiwa hospitalini na kupona.

Sauti Mlimila.

Pamoja na hayo nae mganga mkuu wa wilaya ya Kongwa Dkt Thomas Mchomvu amesema kuwa Kijiji Cha Ngomai kimekuwa na sifa nzuri ndani ya wilaya na kuwa takwimu za mwezi wilaya huzalisha watoto 1300 hadi 1400 ambapo kati yao watoto 30 hadi 40 huzaliwa katika zahanati ya Kijiji cha Ngomai na hii ni kazi kubwa inayofanywa na muuguzi wao.