CCM yakerwa kusuasua miradi ya Maji Dodoma
19 November 2023, 11:18 am
Ikumbukwe kwamba mwezi June mwaka huu, Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi Comredi Daniel Chongolo alifanya ziara Mkoani Dodoma na kuagiza kukamilishwa haraka kwa mradi wa maji wa kata ya chali na Ibihwa lakini mpaka sasa miradi yote imesimama kutokana na kukosekana kwa fedha za kukamilisha miradi hiyo.
Na Bernad Magawa.
Kamati ya Siasa ya Chama cha mapinduzi Mkoa wa Dodoma imesikitishwa na kukwama kwa miradi ya maji inayotekelezwa ndani ya wilaya za mkoa huo na kuahidi kufuatilia kwa undani chanzo cha kutokamilika kwake ili wote wanaohusika kukwamisha miradi hiyo waweze kuwajibishwa.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa Itikati Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Dodoma Bw. Jawadu Mohamed wialayani Bahi wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipofika kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kamati hiyo ndani ya mkoa mzima wa Dodoma kuona na kukagua miradi yote iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa.
Akizungumza na baadhi ya viongozi wa chama na Serikali baada ya kukagua Miradi ya maendeleo wilayani Bahi ukiwemo mradi wa maji katika kata ya chali unaotarajia kugharimu Bilion 2.3 mpaka kukamilika kwake Bw. Jawadu Mohamed amesema chama hakiwezi kuona wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa maji wakati kiliahidi kusogeza huduma zote muhimu kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya Siasa Mkoa huo Ndg. Samwel Malechele amesema CCM haiwezi kuvumilia kuona maelekezo ya viongozi wakubwa wa chama yanapuuzwa huku akiwaomba radhi wananchi wa kijiji cha Chali kwa kuendelea kukosa huduma ya Maji.
Awali, akitoa taarifa ya mradi wa maji wa kata ya chali mbele ya kamati ya Sisasa ya Mkoa wa Dodoma, Meneja wa Ruwasa wilaya ya Bahi Mhandisi Robart Mgombelwa amesema Mradi huo ulipaswa kukamilika Mwezi Julai mwaka huu lakini haujakamilika kutokana na kukosekana kwa fedha.