Mkuu wa wilaya Kongwa awabana watendaji wa maji Mtanana
2 November 2023, 11:51 am
Hivi karibuni kikao hicho kilifanyika katika kata ya mtanana hii ni baada ya kubaini uwepo wa harufu ya Ubadhilifu wa Mapato yanayokusanywa kupitia Miradi ya Maji katika Kata hiyo hali iliyopelekea kushamiri kwa matumizi ya fedha mbichi.
Na Mariam Kasawa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema amevitaka vyombo vya Watoa huduma za Maji Kata ya Mtanana kuwasilisha haraka Nyaraka mbalimbali za matumizi ya fedha.
Mapema akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya kupitia kikao cha pamoja na viongozi mbalimbali na vyombo vya watoa huduma za Maji kutoka Kata ya Mtanana na kuhusisha Vijiji vya Chigwingwili, Ndalibo, Mtanana ‘A’ na Mtanana ‘B’ taarifa hiyo ilibainisha ukiukwaji wa kanuni zinazosimamia ukusanyaji wa Mapato .
Mhe. Mwema amewataka Viongozi wa Kata na Vijiji pamoja na Wataalamu wa RUWASA kutimiza wajibu wao na kubaini mapema uwepo wa Ubadhilifu wa namna hiyo na kuchukua hatua mapema.
Taarifa ya Mkaguzi imebaini Kamati hizo kufanya matumizi ya fedha tasilimu (Mbichi) kiasi cha Tsh. 13, 834,335 (Ambapo Kijiji cha Mtanana ‘A’ pekee ni Tsh. 11,030,785 na Tsh. 2,803,550 Kijiji cha Ndalibo), Aidha malipo ya kiasi cha Tsh. 7,752,000.00 yalikosa viambata, Stakabadhi za kukiri na Orodha za walipwaji zilizosainiwa, huku kiasi cha Tsh. 4,271,045.00 bakaa baada ya Matumizi ikiwa ni kiasi kilichopaswa kupelekwa Benki kwa kadri ya Nyaraka lakini hakikuwahi kupelekwa Benki.