Madereva bodaboda wanaoendekeza tamaa Bahi waonywa
25 October 2023, 1:25 pm
Bodaboda wamekuwa na mazoea ya kukodiwa usiku wa manane na watu ambao hawawafahamu matokeo yake wanauawa na kuporwa pikipiki.
Na. Bernad Magawa.
Kamanda wa Polisi wilaya ya Bahi SSP Idd Ibrahim amekemea vikali madereva wa bodaboda wanaoendekeza tamaa ya fedha kwa kukodiwa na watu wasiowafahamu kwa ahadi ya kulipwa ujira mkubwa huku akiwakumbusha wananchi kuacha kuhifadhi wageni wasiowafahamu bila kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali.
Akizungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bahi sokoni SSP Idd Ibrahim amesema bodaboda wamekuwa wakijali fedha kuliko uhai wao jambo ambalo ni hatari.
Aidha amesema bodaboda wamekuwa na mazoea ya kukodiwa usiku wa manane na watu ambao hawawafahamu matokeo yake wanauawa na kuporwa pikipiki huku akieleza mbinu wanazopaswa kuzitumia kabla ya kuamua kukodiwa hasa nyakati za usiku.
SSP Idd Ibrahim pia amewaeleza wananchi madhara ya kuwapa hifadhi wageni wasiowafahamu huku akikemea vikali watu wanaonunua simu janja zilizotumika na kusema kuwa kwa sasa ni hatari na wanaweza kufungwa kupitia simu hizo bila hatia.