Wananchi Membe waomba semina zaidi mradi wa bwawa
13 September 2023, 5:46 pm
Mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji unatarajia kuchukua takribani hekari 8000 ambapo ndani yake ndipo yanapatikana mashamba ya wananchi wanao hitaji kufahamu hatima ya mashamba hayo.
Na Victor Chigwada.
Uelewa wa wananchi wa Kijiji cha Membe wilayani chamwini kuhusu Mradi wa bwawa la umwagiliaji linalotekelezwa kijijini hapo bado upo chini hali iliyowalizimu wananchi hao kuomba semina zaidi
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesema wamekuwa na mkanganyiko kuhusu Mradi huo kutokana na kuachwa nyuma katika hali ya ushirikishwaji wa kila hatua ya utekelezwaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa hilo
Aidha wamesema licha ya jitihada za kuendelea kufuatilia na kutaka kufahamishwa juu ya nini kinaendelea katika mradi huo lakini wameshindwa kupewa majibu ya kujitosheza kutoka kwa viongozi wa kijiji hadi ngazi ya Kata.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chitabuli Kata ya Membe Bw.Keneth Msindwa amekiri wananchi wa kijiji chake na vijiji jirani wamekuwa na uhitaji wa majibu ya kutaka kufahamu hatima ya mashamba yao yanayo twaliwa kwaajili ya mradi huo.
Msindwa amesema kuwa kukosekana kwa maelezo ya kutosha juu mradi huo imekuwa kero kwa wananchi na kuiomba Serikali kupitia Wizara husika kulitilia maanani jambo hilo.