Wazazi, walezi watakiwa kutowaficha watoto wenye ulemavu
31 July 2023, 6:33 pm
Jamii imeendelea kusisitizwa kutowaficha watoto wenye changamoto ya ulemavu wowote bali iwaweke wazi ili waweze kupatiwa mahitaji ya msingi ikiwemo elimu.
Na Pius Jayunga.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha watoto wao ndani akisema kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za msingi.
Mhe. Ummy ametoa kauli hiyo katika ziara yake alipotembelea wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwanga Viziwi, wilaya ya Same pamoja na wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa watu wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine hivyo inapaswa kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na fursa ili waweze kujikwamua kiuchumi na kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Naye mkuu wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro Mhe. Abdallah Mwaipaya ameishukuru serikali kwa kuanzisha shule za watu wenye ulemavu kwani hutoa fursa kwao kupata ujuzi na stadi za maisha.
Akitoa taarifa ya watu wenye ulemavu katibu wa Shirikisho la Vya vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro Bwn. Jeremia Shayo ameeleza kwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa viungo bandia pamoja na wakalimani wa lugha ya alama katika baadhi ya taasisi hivyo kukwamisha mawasiliano.