Waziri Mhagama akabidhiwa kipande cha sehemu ya ujenzi wa uwanja wa Mashujaa
3 July 2023, 3:35 pm
Mwakilishi wa kampuni ya Ujenzi kutoka SUMA JKT kanda ya Kati Meja Samweli Jambo, amesema ujenzi huo umefuata taratibu zote za upimaji na viwango.
Na Pius Jayunga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amekabidhiwa kipande cha sehemu ya ujenzi wa uwanja wa mashujaa, katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma .
Ujenzi huo unaotekelezwa na kampuni ya SUMA JKT, Umekamilisha kipande cha sehemu ya kwanza ya ujenzi wa uwanja wa Gwaride ambao unategemewa kutumika katika Maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Julai 25, 2023.
Serikali itahakikisha mnara pamoja na uwanja wake vinakuwa vivutio vya kipekee jijini Dodoma
Akiwa kiwanjani hapo Waziri Mhagama aliesema, Serikali pamoja na kuhamia Dodoma imejenga miundombinu yenye hadhi ya makao Mkuu ya Serikali, na jamii inashuhudia majengo ya Serikali makubwa na miondombinu mingine ikiendelea kukamilishwa.
Akiongelea Ujenzi wa Uwanja huo, Waziri Mhagama amesema, ujenzi utakapo kamilika utakuwa ni wa mfano Barani Afrika.
Kwa Upande Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema uwanja huo utakapokamilika utaongeza uzuri na ubora wa Jiji la Dodoma na Serikali itahakikisha mnara pamoja na uwanja wake vinakuwa kivutio cha kipekee.
Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Katibu wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Serikali kuhamia Dodoma Bw. Meshach Bandawe, amesema ujenzi huo umezingatia suala la mpango kabambe wa ujenzi wa Mji wa Serikali.