Jumuiya ya wazazi CCM Bahi yalaani ndoa za jinsia moja
28 April 2023, 2:00 pm
Maadhimisho hayo yalianza kwa kutoa elimu ya malezi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Bahi ambapo wanafunzi walisisitizwa kuhusu nidhamu na bidii katika masomo.
Na Bernad Magawa.
Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi wilaya ya Bahi imetoa tamko la kulaani vikali ndoa za Jinsia moja na kuwashauri wazazi na walezi kukazia suala la malezi katika familia ili kuwa na taifa lenye hofu ya Mungu na maadili bora.
Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo wilaya ya Bahi Yohana Mgomi katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya wazazi wilaya ya Bahi yaliyofanyika katika ofisi za ccm wilayani humo hapo jana.
Akizungumza katika maadhimisho hayo katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Bahi Paulina Bupamba amewaasa wazazi kukemea mambo yote yanayoharibu maadili ya watoto na kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu.
Awali maadhimisho hayo yalianza kwa kutoa elimu ya malezi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Bahi ambapo wanafunzi walisisitizwa kuhusu nidhamu na bidii katika masomo na baadae kuendelea na elimu mbalimbali ambapo viongozi wengine na wanachama wakaeleza mambo mbalimbali.