Maji safi na salama changamoto kata ya mkonze
26 May 2021, 12:45 pm
Na; Mindi Joseph
Wakazi wa mtaa wa Zinje Kata ya Mkonze jijini Dodoma wameiomba Serikali kuwapelekea maji safi na salama ili kuokoa afya zao kutokana na kutumia maji wanayochimba kwenye korongo ambayo si safi na salama.
Taswira ya habari imezungumza na wakazi hao ambapo wamebainisha kuwa maji ni uhai lakini hadi sasa Mtaa huo licha ya kuchimbiwa kisima kimoja lakini bado hakifanyi kazi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Zinje Bw.Gladife Daudi Samweli amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali za kuchimba visima lakini havifanyi kazi hivyo ufuatiliaji wa makini unahitajika.
Wakati Mtaa wa Zinje ukikabiliwa na changamoto hiyo Tayari Jumla ya Shilingi bilioni tano zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kutatua na kupunguza adha ya maji katika Mkoa wa Dodoma Fedha ambazo zinatumika kuboresha miundombinu ya maji, ambapo hadi sasa tayari visima 10, vimechimbwa vitatu kati ya hivyo vikiwa ni vikubwa na kimoja kitakua na uwezo wa kuchukua lita laki nne kwa saa.