Jamii yatakiwa kutambua kuwa haki sawa katika malezi itapunguza ukatili wa kijinsia
21 April 2021, 10:44 am
Na; Thadei Tesha.
Jamii imetakiwa kuhakikisha inatoa haki sawa katika malezi kwa watoto wao wa kike na wakiume ili kuleta usawa wa kijinsia na kupunguza vitendo vya ukatili kwenye jamii.
Wito huo umetolewa na afisa ustawi wa jamii Dodoma Bi.Faudhia Shukuru Mohamed alipokuwa akizungumza na Dodoma Fm ambapo amewataka wazazi kuwalea watoto wao bila ubaguzi ili kujenga jamii yenye usawa.
Bi.Shukuru amesema wamejitahidi kutoa elimu katika jamii ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini bado kwa Mkoa wa Dodoma vinaendelea katika baadhi ya maeneo.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi jijini hapa wamesema elimu zaidi inahitajika katika jamii zao ili kupunguza vitendo hivyo.
Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikishamiri katika baadhi ya jamii nchini ambapo vimesababisha madhara mbalimbali huku baadhi ya mila na desturi zikitajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa.