Dodoma FM
Dodoma FM
13 February 2026, 5:23 pm

kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi, pamoja na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na kuyaunganisha maeneo yenye uzalishaji mkubwa.
Na Mariam Kasawa.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iko tayari kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Shoroba za Kilimo, Mifugo na Uvuvi (AMP 2050) utakaosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa kati wa juu kwa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uhamasishaji wa ukuzaji na uendelezaji wa shoroba za kilimo uliofanyika mkoani Singida, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mpango huo kwa wataalam wa mikoa na halmashauri, hususan kuhusu dhana ya shoroba za kilimo.
Aidha, ameongeza kuwa mpango huo unalenga kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji ili kuongeza thamani ya mazao, kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi, pamoja na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na kuyaunganisha maeneo yenye uzalishaji mkubwa na miundombinu muhimu kama barabara, reli, bandari, masoko na viwanda vya kuchakata mazao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), Bi. Elizabeth Missokia, amesema kuwa dhana ya shoroba za kilimo ni moja ya miradi ndani ya mpango kabambe wa mageuzi ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, unaounganisha uzalishaji, usindikaji, uchakataji, usafirishaji na uhifadhi pamoja na masoko ili kuharakisha mageuzi ya sekta hizo.