Dodoma FM
Dodoma FM
11 February 2026, 3:50 pm

Kupitia mfumo huo wa kidijitali, wafanyabiashara na wakulima wataweza kutunza kumbukumbu zao za biashara kwa urahisi, kupanua wigo wa masoko, na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia mnyororo mzima wa thamani wa kilimo.
Na Anwary Shaban
Takribani asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo kama mhimili mkuu wa uchumi wao.
Hayo yamedhihirishwa leo katika uzinduzi wa mfumo wa Kilimo Bando uliofanyika jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kuongeza ajira na kurahisisha huduma kwa wakulima nchini.
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa AGRA, Vian, amesema kuwa Kilimo Bando ni mradi unaodhaminiwa na Taasisi hiyo kupitia mpango wa kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na wakulima wasiopungua milioni tatu, sawa na asilimia 65 ya wakulima nchini. Amesema mfumo huo utasaidia kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Kwa upande wake, Muanzilishi wa Bizy Tech ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mahmoud Shoo, amesema mfumo wa Kilimo Bando utarahisisha upatikanaji wa masoko, mbegu bora na pembejeo nyingine za kilimo, huku ukipunguza gharama na umbali ambao wakulima walilazimika kusafiri kufuata huduma hizo.
Naye mmoja wa mawakala wa pembejeo za kilimo (Agro Dealer), Benedikt Masasi, ameishukuru Bizy Tech kwa kuanzisha mfumo huo wa kidijitali, akisema kuwa utarahisisha biashara za kilimo na kuongeza tija kwa wakulima na wafanyabiashara wa sekta hiyo.
Sambamba na hayo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara kutoka Benki ya CRDB, Shabani Maregesi, amesema ushirikiano wao na Bizy Tech utawezesha wakulima kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi katika maeneo yao, hatua itakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo na biashara ndogondogo vijijini.