Dodoma FM

COP 30: Kilimo funika, tumaini jipya kwa wakulima wa maeneo kame

11 February 2026, 12:13 pm

‎Moja ya mbinu zinazozidi kuwasaidia wakulima ni kilimo funika, hususan kulima mazao ya jamii ya mikunde kama choroko.Picha na Asha Kamata.

‎‎Kadri dunia inavyoelekea COP 30, simulizi za wakulima wa Kongwa na kijiji cha Chololo zinaendelea kuonyesha kuwa suluhisho la mabadiliko ya tabianchi lipo mashambani. Kinachohitajika sasa ni uwekezaji katika teknolojia rafiki kwa wakulima, ili mbinu hizi endelevu ziweze kutumika kwa upana zaidi.

Na Mariam Kasawa.
‎Wakati dunia ikiendelea kujadili hatma ya sayari katika majukwaa ya kimataifa kama COP 30, sauti za wakulima wa maeneo kame nazo zinazidi kupata uzito. Katika mikoa inayokabiliwa na mvua chache kama Dodoma, suluhisho la mabadiliko ya tabianchi halisubiri teknolojia za gharama kubwa, bali linachipuka moja kwa moja mashambani.

‎Moja ya mbinu zinazozidi kuwasaidia wakulima ni kilimo funika, hususan kulima mazao ya jamii ya mikunde kama choroko na fiwi. Mazao haya hufunika ardhi, kusaidia kuhifadhi unyevunyevu wa udongo na kupunguza upotevu wa maji, hali inayowezesha mimea kustahimili vipindi virefu vya ukame.
‎Mbali na hilo, wakulima wamekuwa wakitumia mashimo maarufu kama chololo. Mashimo haya huchimbwa kwa mfumo maalum ambapo sehemu ya chini huwekwa juu na ya juu chini.

‎Wakati mvua inaponyesha, maji hayasambai hovyo bali hukusanyika na kubaki ndani ya shimo, hivyo kufyonzwa polepole na udongo na kutumika kwa muda mrefu na mazao.
‎Katika maeneo yenye mwinuko, matuta funika yamekuwa ngao muhimu dhidi ya upotevu wa maji na udongo.

‎Kwa kawaida mvua ikinyesha katika maeneo haya, maji pamoja na udongo huteremka kwa kasi na kuacha mashamba yakiwa tupu.

‎Matuta funika huzuia hali hiyo kwa kufyonza maji, kuyahifadhi na kulinda rutuba ya ardhi. Matuta haya hulimwa kwa mtindo unaofanana na kilimo cha viazi, ambapo udongo wa chini huletwa juu na wa juu kubaki chini, hivyo kusaidia kuhifadhi unyevu.

‎‎Akizungumzia changamoto zilizopo, Mtafiti na Meneja kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) – tawi la Hombolo, Emmanuel Chilagane, anasema kuwa japokuwa mbinu hizi zimewasaidia wakulima wengi kukabiliana na ukame na kuongeza mavuno, zinahitaji nguvu kazi na gharama kubwa, hasa kwa wakulima wenye mashamba makubwa.

Sauti ya Emmanel Changile

‎‎“ Kwa wakulima wadogo mbinu hizi zinaweza kufanyika kwa kutumia jembe la mkono, lakini kwa wakulima wakubwa hali huwa tofauti.

Hawezi kuweka matuta au mashimo kwenye shamba la hekari moja au Zaidi itachukua muda mrefu na gharama itakuwa kubwa Hivyo, kuna umuhimu wa kupatikana kwa mashine ndogo na za bei nafuu zitakazowasaidia wakulima kuchimba mashimo ya chololo na kutengeneza matuta funika kwa wepesi na kwa gharama ndogo zaidi, Kwa kufanya hivyo, mbinu hizi zitakuwa rahisi kutekelezwa kwa wakulima wengi na kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za taifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi”.Alisisitiza Emmanuel Chilanga Meneja TARIHombolo.

‎‎Ashura Ally Mtafiti wa masuala ya udongo kutoka wilaya ya Kongwa anasema mwitikio wa wakulima bado ni mdogo wakulima waliopokea mbinu hizo ni wachache hivyo huwa wanaweka mashamba darasa siku ya wakulima nanenane kwa ajili ya wakulima kujifunza japokuwa mwitikio bado mdogo.

Sauti ya Ashura Ally.