Dodoma FM
Dodoma FM
14 August 2025, 5:01 pm

Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika haya ili kuimarisha ubora wa huduma, kuendeleza mshikamano wa kijamii, na kuchochea maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Na Mariam Matundu.
Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali (NGOs), yanatekeleza shughuli zake kwa uhuru na kuzingatia malengo, mipango, mikakati na vipaumbele vya kitaifa, sambamba na misingi ya uwazi na uwajibikaji.
Dkt. Mpango ameyasema hayo katika hotuba yake iliyowasilishwa kwa niaba yake na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye kilele cha Kongamano la NGOs 2025, Agosti 13, 2025.
Ameeleza kwamba ni ukweli usiopingika kuwa NGOs zimekuwa zikichagiza jitihada za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali hususani katika sekta ya afya, kilimo, elimu,maji, mazingira, utawala bora, ulinzi wa jamii,uwezeshaji wa jamii, miundombinu, mifugo na uvuvi pamoja na sekta nyingine mtambuka.

Dkt. Mpango pia ameeleza kufarijika na ushirikishwaji wa Baraza kikamilifu katika mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, utoaji wa maoni kuhusu sheria za kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), utoaji wa maoni kuhusu mahitaji ya kikodi ya Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwenye Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema kuwa kufanyika kwa Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kumeongeza uelewa na maarifa ya washiriki kupitia mafundisho, mada mbalimbali zilizojadiliwa pamoja na mijadala iliyofanyika.

Awali akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amewashukuru na kuwapongeza wadau mbalimbali wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha utoaji wa huduma bora kwa jamii, pamoja na kuchangia maendeleo na hata uchumi wa Taifa.
clip mwanaidi