Wananchi Ihumwa A waomba kutengewa eneo la kuhifadhi taka
7 November 2023, 5:13 pm
Hali hii inashangaza kuona mtaa huo ambao haupo mbali na ulipo mji wa serikali ukikosa mzabuni wa kukusanya takataka na wananchi wakichoma takataka katika maeneo yao wakati sheria zipo na miongozo ya udhibiti na utunzaji wa mazingira .
Na Victor Chigwada.
Wananchi wa mtaa wa Ihumwa A wameiomba serikali ya mtaa huo kuwatengea eneo la kuhifadhi takataka ili kuepuka mfumo wa kila mmoja kukusanya taka eneo lolote.
Taswira ya Habari imezungumza na wananchi wa mtaa mmojawapo wa kata hiyo kufahamu ni hatua zipi wanatumia kuhakikisha mtaa wao unakuwa safi kila wakati.
Baadhi yao wamesema ni muhimu serikali za mitaa kutenga maeneo ya kuhifadhi takataka kwani njia mojawapo ya kuongeza hali ya Usafi katika maeneo yao.
Aidha wamesema kuwa wamekuwa wakitumia Vikundi na Watu binafsi kubeba Takataka lakini changamoto imekuwa ni wapi taka hizo zinaenda kukusanywa ili kuepusha uchafuzi wa mazingira kwa wakati mwingine.
Vilevile wamesema kukosekana kwa eneo maalum la kukusanyia takataka imesababisha baadhi ya watu kutupa takakata kwenye Mitaro ya Maji na maeneo ya makazi ya watu.
Taswira ya Habari imeutafuta Uongozi wa Mtaa wa Ihumwa A kwa ajili ya kupata Ufafanuzi wa changamoto hiyo ambapo Mwenyekiti wa mtaa huo Bw. Wiliamu Njilimuyi amekiri kuwa mtaa huo hauna sehemu maalumu ya kukusanyia Takataka kutokana na eneo ambalo lilikuwa likitumika awali kusitishwa.
Mwenyekiti huyo amesema ni vema wananchi kuendelea kutunza takataka na wakati mwingine kuzichoma katika maeneo yao wakati serikali ya mtaa huo ikiendelea kusubiri mzabuni wa ukusanyaji wa Takataka apatikane.
Ikumbukwe kuwa Ihumwa A ni moja ya mitaa inayopatikana katika Halmashauri ya jiji la Dodoma ambapo ndani ya Halmashauri hiyo kuna idara ya Mazingira ambapo jukumu lao mojawapo ni Kusimamia usafi na uhifadhi wa Mazingira katika maeneo yote ya mipaka ya Jiji la Dodoma ikiwemo udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira katika makazi,viwandani, mahotelini, maeneo mbalimbali ya kibiashara.