Wanawake Bahi watakiwa kusimamia maadili ya watoto
18 July 2023, 12:52 pm
Mbunge wa Bahi amesema kipaumbele chake ni kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa salama.
Na Bernad Magawa.
Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Fatuma Taufiq amewaasa wanawake wilayani Bahi kusimamia maadili ya watoto ili kutokomeza viashiria vya maadili mabovu yanayopelekea uwepo wa ndoa za jinsia moja na unyanyasaji wa kijinsia.
Akizungumza kupitia baraza la wanawake wa CCM wilaya ya Bahi (UWT) Mheshimiwa Taufiq pia amewakumbusha kinamama kuwasaidia wasichana waliopata ujauzito wakiwa shule warudi masomoni ili wapate fursa ya kutimiza ndoto zao.
Naye Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Bahi Imakulata Masigati akizungumza katika baraza hilo ameahidi kushirikiana na wanawake wilayani humo katika kazi za maendeleo.
Akieleza namna anavyopambana kuboresha miundombinu ya afya wilayani Bahi ili kuwahakikishia usalama wanawake wakati wa kujifungua, Mbunge wa jimbo la Bahi Mheshimiwa Kenneth Nollo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika baraza hilo amesema kipaumbele chake ni kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa salama.