BOOST kuboresha elimu kongwa
19 April 2023, 2:20 pm
Mradi wa BOOST ulianzishwa na Serikali chini ya ufadhili wa benki ya dunia unaosimamiwa na ofisi ya Rais TAMISEMI utatumia zaidi ya bilioni 1 na milioni 352 kutekeleza ujenzi huo ambao ni moja ya afua zake.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Mradi wa BOOST unatarajia kujenga shule mpya mbili vyumba vya madarasa vilivyokamilika 26 vyoo 18 na darasa la elimu maalum moja katika shule za msingi na awali wilayani Kongwa.
Hayo yameelezwa na Mwalimu Magreth Temu Afisa Elimu Awali na Msingi wilaya ya Kongwa wakati akielezea kwa ufupi taarifa ya maandalizi ya utekelezaji wa ujenzi kupitia mradi wa BOOST ambapo amesema ujenzi huo utafanywa katika shule za msingi 9 za wilayani humo zikiwemo Ihanda juu, Mtanana, Tubugwe, Wangazi na shule mpya ya Moleti.
Akipokea taarifa hiyo mbele ya wajumbe wakiwemo kamati ya ulinzi na usalama Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel amesisitiza kazi zote za ujenzi zifanywe na mafundi wazawa na vifaa vyote vya ujenzi vinunuliwe kwa wafanyabiashara wazawa wakazi wa Kongwa ili kukuza uchumi wa wananchi wake.
Aidha Mwema ameongeza kuwa viongozi wanatakiwa kushirikisha wananchi katika ujenzi wa miundombinu hiyo na miradi mingine ya maendeleo kwani nguvu za wananchi ni sehemu ya kutekeleza miradi.
Sambamba na hayo nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kongwa Dkt. Omary Nkullo ametilia mkazo suala la ushirikishwaji uwazi na ukweli juu ya taarifa za ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuondoa mashaka kwa wananchi.