Rais Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuzingatia mipango na vipaumbele vya kitaifa.
30 September 2021, 1:22 pm
Na;Mariam Matundu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuzingatia Mipango na Vipaumbele vya Kitaifa katika kutekeleza majukumu na miradi mbalimbali ya maendeleo
Rais Samia amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Mkutano wa Mwaka wa Mashirika hayo.
Aidha, ameyataka Mashirika hayo kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao na miradi mbalimbali kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi za nchi.
Aidha ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhamasisha zoezi la Sensa likatalofanyika nchini mwaka 2022 ili Taifa liweze kujiletea Maendeleo katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza Rais kwa uongozi wake mahiri uliowezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupata uongozi.
Ameongeza pia, kupitia mkutano huo Mashirika hayo yamepata semina elekezi kuhusu sheria, kanuni na miongozo hivyo ni matumaini kuwa sasa wamefahamu wanatakiwa kufanya nini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dkt. Lilian Badi amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yatazingatia sheria, kanuni na miongozo pamoja na kushirikiana na Serikali ili kutoa mchango wenye tija nchini.