Wazee Nchini washauriwa kutumia fursa ya chanjo ili kuimarisha kinga dhidi ya miili yao
4 August 2021, 12:10 pm
Na; Mariam Matundu.
Wazee nchini wameshauriwa kutumia fursa ya chanjo dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Korona UVIKO 19 ili kuimarisha kinga ya miili yao kipindi hiki ambacho Serikali imewapa kipaumbele.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati akizungumza na Wajumbe wa Chama cha Wanasheria wanawake Nchini TAWLA waliomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma ambapo amesisistiza ushiriki wa makundi mbalimbali katika kupambana na UVIKO19.
Ameongeza kuwa Wazee ni tunu ya Taifa hivyo Jamii ina wajibu wa kuwalinda na majanga mbalimbali ikiwemo kuimarisha usalama wa Afya zao.
Aidha, Dkt. Jingu amewataka Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wote kuhakikisha Wazee wanaokwenda kupata chanjo kwenye vituo katika maeneo yao wanapata huduma zote wanazostahili bila usumbufu wa aina yoyote.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa Chanjo hapa nchini tarehe 28 Julai, 2021ambapo kwa mkoa wa Dodoma zoezi hili limezinduliwa jana Agost 3 .