Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Konde
3 June 2021, 1:36 pm
Na; TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Konde na Udiwani katika Kata Sita za Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 18 Julai mwaka 2021.
Akitangaza uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo Dkt. Wilson Mahera Charles amesema uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Konde lililopo Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba, umekuja kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Khatib Said Haji kufariki dunia.
Amesema tayari Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaitaarifu NEC juu ya kuwepo wazi kwa nafasi hiyo kama inavyoelekezwa na Kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.
Dkt. Charles ameongeza kuwa Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara.
Amezitaja kata hizo kuwa ni Kata ya Mbagala Kuu iliyopo Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Kata ya Ndirigishi iliyopo Wilaya ya Kiteto mkao wa Manyara, Kata ya Mitesa iliyopo Wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara, Kata ya Gare iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoa wa Tanga, Kata ya Mchemo iliyopo Wilaya ya Newala mkoa wa Mtwara na Kata ya Chona iliyopo Wilaya ya Ushetu mkoa wa Shinyanga.
Akizungumzia kuhusu ratiba ya uchaguzi huo mdogo, Dkt. Charles amesema fomu za uteuzi zitaanza kutolewa kuanzia tarehe 21 Juni hadi tarehe 27 Juni mwaka 2021, uteuzi utafanyika tarehe 27 Juni mwaka 2021, wakati kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 28 Juni hadi tarehe 17 Julai mwaka 2021 na siku ya kupiga kura itakua tarehe 18 Julai mwaka 2021.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayri imeshavifahamisha vyama vya siasa juu ya uchaguzi huo mdogo ili kuwasilisha majina ya wagombea watakaoshiriki katika Uchaguzi huo.