Dodoma FM
Dodoma FM
26 March 2026, 17:23

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha usawa wa fursa za elimu kwa watoto wote, hususan wale wenye mahitaji maalum, na kuendelea kujenga jamii inayojali na kujumuisha kila mwananchi.
Na Mariam Kasawa.
Afisa Elimu Maalum Jiji la Dodoma, Mwl. Issa Kambi, amekabidhi rasmi taarifa ya zoezi la ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum kwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dkt. Pima Sebastian, katika hatua muhimu ya kuimarisha huduma za elimu jumuishi.
Zoezi hilo la ubainishaji lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma limepata watoto 328 ambao wamebainishwa ikiwa na lengo la kutambua watoto wenye mahitaji maalum, wakiwemo wenye ulemavu wa aina tofauti pamoja na changamoto za kujifunza ili waweze kupatiwa msaada stahiki wa kielimu na kijamii.
Akikabidhi taarifa hiyo, Mwl. Kambi alieleza kuwa matokeo yanaonesha uwepo wa idadi kubwa ya watoto wanaohitaji uangalizi na mipango maalum ili waweze kunufaika kikamilifu na haki yao ya kupata elimu.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, walimu, wataalamu wa afya pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika kuhakikisha watoto hao wanapatiwa mazingira rafiki ya kujifunzia.

Aliongeza kuwa takwimu zilizokusanywa zitasaidia Jiji kupanga mikakati madhubuti ya kuboresha miundombinu ya shule, kuongeza walimu wa elimu maalum pamoja na upatikanaji wa vifaa saidizi.
Kwa upande wake, Dkt. Pima Sebastian alipokea taarifa hiyo na kuipongeza timu ya elimu maalum kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Aliahidi kuwa Jiji litatumia taarifa hiyo kama nyenzo muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya kuboresha huduma za elimu jumuishi, sambamba na kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.