Dodoma FM

Elimu ya itifaki yasisitizwa Dodoma

03/03/2026, 16:38

Picha ni Mkuu wa mkoa akiwa amefika katika mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa na ‘The Embassy of Protocol ‘katika ukumbi wa Zabibu Hotel, Jijini Dodoma.Picha na Mkoa wa Dodoma.

“Dhamira yetu ni kujenga utamaduni wa kuzingatia itifaki katika sekta zote na kuhakikisha huduma hii inawafikia watumishi wengi zaidi,” amesema Sijabeja.

Na Mariam Kasawa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amezitaka taasisi za Serikali na Binafsi kuwapeleka Maafisa Habari na watumishi wa kada nyingine kupata mafunzo ya itifaki ili kuongeza weledi na ufanisi katika utendaji kazi.

Akizungumza Machi 02, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa na ‘The Embassy of Protocol ‘katika ukumbi wa Zabibu Hotel, Jijini Dodoma.

Mhe. Senyamule amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kujenga taswira chanya ya taasisi na kuimarisha mahusiano ya kikazi.

“Itifaki ni msingi wa nidhamu, heshima na mpangilio sahihi wa shughuli za taasisi. Ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha watumishi wake wanapata elimu hii muhimu,” amesisitiza Mhe. Senyamule.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ‘The Embassy of Protocol’ Bw. Sharbely Sijabeja, amesema taasisi hiyo imefikisha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake na itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa ofisi na taasisi mbalimbali Nchini.