Dodoma FM
Dodoma FM
29 January 2026, 1:34 pm

Picha ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba , Bungeni jijini Dodoma. Picha na Wizara ya Afya.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuboresha na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, sambamba na kuimarisha usimamizi wa viwango vya gharama za huduma za matibabu, ili kuhakikisha huduma za afya zinakuwa nafuu, bora na zinazomudu kwa Watanzania wote.
Na Mariam Kasawa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza wizara ya afya na taasisi zinazohusika na sekta ya afya kuhakikisha zinazingatia na kusimamia kikamilifu viwango vya serikali vya utoaji wa huduma za afya, ili kulinda maslahi ya wananchi na kuwawezesha Watanzania kumudu gharama za matibabu.
Dkt. Nchemba ametoa maelekezo hayo leo Januari 29, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mhe. Emmanuel Cherehani, aliyewasilisha malalamiko ya wananchi wanaokwenda kupata huduma za matibabu na kulazimika kulipa fedha za kumuona daktari bila kuwepo kwa viwango vya uwiano vinavyoeleweka.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema serikali imedhamiria kuweka na kusimamia viwango vya matibabu vinavyoeleweka na vinavyofanana nchi nzima, ili kuondoa utofauti wa gharama kati ya hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya, hali inayowaumiza wananchi na kuchelewesha upatikanaji wa huduma.
Amesema uwepo wa mifumo na taratibu zilizo wazi katika utoaji wa huduma za afya ni jambo la msingi katika kudhibiti gharama na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati na kwa gharama zinazomudu.
Aidha, Dkt. Nchemba amefafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, mfumo wa huduma za afya nchini umejengwa katika dhana ya kuchangiana gharama za matibabu kupitia vifurushi mbalimbali vilivyoainishwa kisheria, ili kila Mtanzania aweze kupata huduma za afya bila kikwazo cha kifedha.
Ameongeza kuwa wananchi ambao hawajajiunga na bima ya afya wanatakiwa kuchangia gharama za huduma wanazopata katika hospitali za umma, isipokuwa kwa makundi maalum yaliyotambuliwa kisheria ambayo yamesamehewa kuchangia, ikiwemo wazee wasio na uwezo, watoto na makundi mengine maalum.